Swift

KANISA LISILOONEKANA KWA MACHO YA NYAMA




UTANGULIZI
Wakristo wengi hupenda kutambulika katika madhehebu yao. Hupenda kutambulika katika Makanisa au Ushirika wao lakini wamesahau kutambulika katika Kanisa Lisiloonekana. Unaweza ukatambulika katika Ushirika au Kanisa fulani kwa jina lake lakini usitambulike katika Kanisa Lisiloonekana. Ni Wakristo wachache wanaotambulika katika Kanisa Lisiloonekana. Ni makusudi ya somo hili kuweza kujitambua binafsi kwamba upo kwenye Kanisa lipi?
MAANA YA KANISA
Neno Kanisa kwa kiyunani ni "EKKLESIA" ambalo lina maana ya wao walioitwa na kutolewa kati yao au kusanyiko. Mkusanyiko wa watu walioitwa na kutolewa kati yao. Mkusanyiko wa waaminio walioitwa na kutolewa kati ya watu wengine.
Matendo 7:37-38
“Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye. Yeye ndiye aliyekuwa katika KANISA JANGWANI pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi.”
‭‭
KANISA LINALOONEKANA 
Hili ni Kanisa ambalo waamini au wale walioitwa na kutolewa kati yao huenda kushiriki au kukusanyika pamoja kwa ajili ya kumfanyia Bwana ibada. Hapo ndipo tunapokuwa na mikusanyiko mbalimbali mikubwa kwa midogo kwa lengo la kumuabudu Mungu. Majina ya madhehebu ndipo yanapoonekana kwa sura hii. Utajitambulisha kwamba umetokea Kanisa gani iwe TAG, EAGT, GMI, FPCT, KLPT na mengineyo mengi tu. Ni vizuri kutambulika katika Kanisa linaloonekana lakini ni vizuri zaidi kutambulika kwanza katika Kanisa Lisiloonekana.
Matendo 10:25
“wala tusiache KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”
Kila mtu aliyeokoka ni lazima awe na mahali ambapo anatambulika kwamba yeye ni mshirika au muumini wa Kanisa hilo ili aweze kupewa huduma za kichungaji. Kila mmoja lazima awe na Mchungaji mwanadamu ambaye atakuwa akimchunga na kulishwa neno la Mungu.
Matendo 13:1-2
“Na huko Antiokia katika KANISA lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa WAKIMFANYIA BWANA IBADA na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.”
‭‭
Nyakati hizi tulizonazo wapo Wapendwa ambao hawataki kuchungwa na kuwepo katika Kanisa linaloonekana kwa ajili ya huduma za Kichungaji. Wengine wao wanaishia kwenye TV tu na kusema watasali kwa njia hiyo hawana haja ya Mchungaji, ukimsikia mtu wa namna hiyo ujue huyo siyo "KONDOO" bali ni "MBUZI". Ni ngumu sana kumchunga mbuzi ukimletea chakula karibu utaona ataruka ruka akaparamie kisamvu mahali. Ndiyo maana mbuzi hufungwa kamba siyo kondoo. Jiulize wewe ni mbuzi au kondoo. Iwapo hauna sehemu ambayo wewe ni mshirika hapo bali unazunguzunguka tu ujue una tabia za mbuzi.
‭KANISA LISILOONEKANA
Kanisa hili ni Kanisa ambalo linalojumlisha watu wote waliookoka ambao majina yao YAMEANDIKWA Mbinguni. Kanisa hili pia huitwa Kanisa la Wazaliwa wa Kwanza. Hapo sasa haliangaliwi dhehebu la mtu husika ili mradi tu jina lake lipo kwenye Kitabu cha Uzima Mbinguni. Jina lako linaweza likawepo katika daftari la Kanisa linaloonekana lakini lisiwepo katika Kitabu cha uzima au katika Kanisa Lisiloonekana.
Waebrania 12:22-23
“Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na KANISA LA WAZALIWA WA KWANZA WALIOANDIKWA MBINGUNI, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika,”
Wako baadhi ya watu wanaishia kwenye Ibada za mitandaoni tu lakini hawana mahali ambapo wamejisajili katika Kanisa linaloonekana hilo ni KOSA ni lazima tuwepo mahali ambapo tunapata huduma za Kichungaji.
1 Petro 1:1
“Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa WATEULE WA UTAWANYIKO, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia;”
Hili ni Kanisa ambalo limetawanyika kote Duniani ambalo pia waumini wake huitwa WATEULE wa Utawanyiko. Wameteuliwa na Mungu kuweza kuirithi Mbingu. Majina yao yako Mbinguni.
JINSI YA KUWA KATIKA KANISA LISILOONEKANA
I. Kutubu dhambi kwa kuziacha
Mithali 28:13
“Afichaye DHAMBI zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na KUZIACHA atapata rehema.”
Ili uweze kuandikwa katika Kanisa lisiloonekana ni lazima utubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wako.

II. Kulitii neno la Mungu
Zaburi 119:9
“Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa KUTII, akilifuata neno lako.”
Ili uendelee kubaki katika Kanisa lisiloonekana ni lazima uwe mtii katika neno la Mungu. Ukiwa muasi katika neno la Mungu unakuwa ni mtoto wa Shetani maana yeye ndiye baba wa uasi. Kila atendaye dhambi afanyavyo uasi mbele za Mungu.
1 Yohana 3:4, 8
“Kila atendaye dhambi, afanya UASI; kwa kuwa dhambi ni UASI.
atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
‭‭
Unasafisha njia yako ya kwenda Mbinguni kwa kulitii neno la Mungu.
III. Kuishi maisha ya Utakatifu
1 Petro 1:15-16
“bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi IWENI WATAKATIFU katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Kuwepo katika Kanisa lisiloonekana kunategemeana na kuishi kwetu katika utakatifu. Majina yetu ufutwa katika kitabu cha Uzima pale tunapodumu kufanya dhambi. Watakatifu ndiyo ambao watakaoweza kumuona Mungu. Kwahiyo tunatakiwa kuishi katika utakatifu hapa Duniani na siyo baada ya kufa. Watakatifu walioko Duniani ndiyo ambao wanaompendeza Mungu.
Zaburi 16:3
“WATAKATIFU waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.”
IV. Kukusanyika Pamoja na wateule wenzako
Waebrania 10:25
“wala tusiache KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”
Majina yetu yakiwapo katika Kanisa lisiloonekana bado tuna wajibu wa kukusanyika pamoja katika Kanisa linaloonekana. Tunawajibika kuwepo katika ushirika wa mahali fulani na kuwa chini ya Mchungaji mwanadamu fulani. Tunakusanyika pamoja ili tuweze kuimarishwa kiroho na kuweza kumzalia Mungu matunda. Haitoshi kusema nitasali kwenye TV bali tuwepo mahali Fulani chini ya Mchungaji fulani.

You Might Also Like

0 comments